Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034)

Dhana ya Nishati Safi ya Kupikia
Kwa mujibu wa Mwongozo wa Benki ya Dunia kuhusu nishati safi ya Kupikia (World Bank Multi-Tier Framework – MTF), wa mwaka 2020, nishati safi ya kupikia hupimwa kwa ufanisi, urahisi wa kutumia, upatikanaji, usalama, unafuu na yenye kiwango kidogo cha sumu. toa ki Vilevile, Mwongozo wa Shirika la Afya Duniani wa mwaka 2021 umeeleza kuwa nishati safi na teknolojia hupimwa kwa viwango vya chembechembe ndogo za vumbi zenye ukubwa usiozidi 2.5µm (PM2.5) na hewa ya kaboni monoksaidi zinazotolewa. Viwango hivyo ni:

i. Wastani wa kiwango cha ubora wa hewa (air quality guideline level, AQG) cha 5 μg/m3 kwa Mwaka  au kiwango cha mkusanyiko wa hewa chafu (interim target) cha 35 μg/m3  kwa Mwaka  kwa  chembe  chembe ndogo za vumbi zenye ukubwa wa 2.5 μm (PM2.5), na

ii. Wastani wa kiwango cha ubora wa hewa (air quality guideline level, AQG) cha 4 mg/m3 kwa saa 24 au kiwango cha mkusanyiko wa hewa chafu (interim target) cha 7 mg/m3 kwa saa 24 kwa kaboni monoksaidi.

Hivyo, kwa muktadha wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, nishati safi ya kupikia ni dhana inayotumika kuelezea na kubainisha nishati na teknolojia sahihi ambapo kwa pamoja hutoa moshi wenye kiwango kidogo cha sumu pale zinapotumika kwa usahihi. Dhana hii ina lengo la kuhakikisha usalama, uendelevu na urahisi wa upatikanaji wa nishati ya kupikia, kuokoa muda, pamoja na kupunguza gharama za matumizi, athari za kimazingira na kiafya kwa watumiaji. Pia, ni nyenzo muhimu katika kutekeleza makubaliano ya kitaifa na kimataifa yanayolenga kupambana na mabadiliko ya tabianchi na kupunguza uzalishaji wa gesi joto.

Chimbuko la Mkakati
Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia unatokana na hitaji la kuwa na mpango jumuishi wa kitaifa katika kukabiliana na ongezeko la uharibifu wa mazingira pamoja na athari za kiafya, kiuchumi na kijamii zinazotokana na matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia. Kutokana na suala la nishati ya kupikia kuwa mtambuka, kumekuwa na changamoto ya utekelezaji wa mikakati ya kupunguza athari hizo. Tangu Tanzania ipate uhuru Mwaka 1961, haijawahi kuwa na mpango jumuishi wa kitaifa wa kupunguza matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia.

Sera ya Taifa ya Nishati ya Mwaka 2015 imeeleza kuwa, ongezeko la matumizi ya nishati ya tungamotaka pamoja na teknolojia zisizo fanisi za kupikia, namna za matumizi ya nishati katika kupika na matumizi ya majiko yasiyo fanisi imechangia katika uharibifu wa mazingira na matatizo ya kiafya yanayohusiana na moshi. Hivyo ni muhimu kutekeleza jitihada za kuhamia katika matumizi ya nishati nyingine kama vile gesi asilia, gesi oevu (LPG) na umeme.

Mkakati huu umeandaliwa ili kutekeleza lengo la Sera ya Taifa ya Nishati ya Mwaka 2015 la kuboresha maisha ya wananchi kupitia matumizi ya nishati za kisasa za kupikia pamoja na matamko ya kisera (i) kuimarisha mabadiliko ya nishati ya kupikia kutoka kwenye kuni na mkaa kwenda kwenye nishati za kisasa; na (ii) kuwezesha matumizi ya majiko na vifaa sahihi vya kupikia ili kukuza matumizi ya nishati safi za kupikia ambazo ni mbadala wa kuni na mkaa.

Pia, utekelezaji wa Mkakati huu utawezesha kufikiwa kwa malengo yaliyowekwa katika Sera mbalimbali za kitaifa, ikiwemo Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021 yenye lengo la kuimarisha uhifadhi wa misitu kwa ajili ya utunzaji wa mazingira kupitia  matumizi ya nishati mbadala zenye gharama nafuu na zinazopatikana kwa urahisi kama vyanzo vya nishati ya kupikia; Sera ya Taifa ya Misitu ya Mwaka 1998 yenye lengo la kuhakikisha upatikanaji endelevu wa mazao na huduma za misitu kwa kudumisha eneo la misitu la kutosha chini ya usimamizi madhubuti;  Sera ya Taifa ya Afya ya Mwaka 2007 inayoelekeza kuwa na utaratibu mzuri na endelevu wa kuhifadhi, kutunza na kulinda mazingira kwa faida ya afya  ya wanachi na vizazi vijavyo; na Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Mwanamke na Jinsia ya Mwaka 2000 inayolenga kutunza mazingira kwa ajili ya kumpunguzia mwanamke mzigo wa kutafuta kuni na maji ili kuwezesha ushiriki wake katika kutekeleza shughuli za kijamii.

Wakati wa  ufunguzi wa Mjadala wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia uliofanyika mwezi Novemba, 2022 , Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alielekeza uandaliwe Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia utakaotoa mwelekeo wa namna ya kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia. Aidha, Mhe. Rais alielekeza kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wawe wamehamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia ndani ya kipindi cha miaka 10.

Hivyo, madhumuni ya Mkakati huu ni kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi, salama, nafuu, endelevu na ya uhakika ya kupikia. Mkakati huu umeainisha mikakati ya utekelezaji, shabaha, viashiria vya matokeo pamoja na wadau watakaokuwa na wajibu wa utekelezaji wa Mkakati huu na majukumu yao. Masuala mengine yaliyoainishwa katika Mkakati ni muda wa utekelezaji pamoja na mpango kazi wa utekelezaji wake.

Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034)_compressed

Related Posts